Jumatano 2 Septemba 2026 - 12:29
Mwanza Kuandika Historia ya Maulidi/ Hafla Kubwa ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa Mtume (s.a.w.w.) Kufanyika Igogo

Hawza/ Wakazi wa jiji la Mwanza na maeneo ya jirani wanatarajiwa kushuhudia hafla kubwa na yenye kuleta furaha ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), katika hafla inayotarajiwa kuwakutanisha Waislamu na wageni mbalimbali katika mazingira ya upendo, mshikamano na kumuenzi Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.).

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hafla hiyo ya Maulidi imeandaliwa na Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Tawi la Mwanza, chini ya usimamizi wa Sheikh Hashim Ramadhani, kwa kushirikiana na taasisi ya The Desk and Chair Foundation.

Kwa mujibu wa maandalizi yaliyofanyika, hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Ijumaa, tarehe 4 Septemba 2026, katika eneo la Igogo kwa Mzee Balichako, kuanzia saa 20:45 usiku hadi saa 00:45, huku hafla hiyo ikitarajiwa kuwa fursa adhimu kwa waumini na wananchi kwa ujumla kukutana kwa ajili ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), kukumbushana mafundisho yake matukufu na kutafakari juu ya nafasi ya ujumbe wake katika kuijenga jamii yenye upendo, amani, mshikamano na maadili mema.

Viongozi na wageni mbalimbali kuhudhuria

Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa dini, wanazuoni pamoja na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mwanza. Miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhudhuria ni Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithnaashariyyah Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala, pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke, sambamba na masheikh na viongozi wengine mbalimbali.

Ushiriki wa viongozi hao unatarajiwa kuifanya hafla hiyo kuwa moja ya mikusanyiko muhimu ya kidini katika jiji la Mwanza, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza utamaduni wa kuadhimisha maisha, mwenendo na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.).

Kumbukumbu ya Mtume; ujumbe wa upendo na umoja

Maadhimisho ya Maulidi ni fursa muhimu ya kumkumbuka Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na kuhuisha mafundisho yake katika maisha ya kila siku, hususan mafundisho yanayohusu upendo, huruma, kusameheana, udugu, kuheshimiana na kuishi kwa amani.

Waandaaji wanatarajia kwamba hafla hiyo itakuwa sehemu ya kuimarisha mahusiano mema miongoni mwa Waislamu na jamii kwa ujumla, huku ikitoa nafasi ya kushirikiana katika kusherehekea kumbukumbu adhimu ya kuzaliwa kwa Mtume wa Rehema (s.a.w.w.).

Kwa hivyo, macho na nyoyo za waumini na wapenda amani zinaelekezwa Mwanza, ambako Igogo inatarajiwa kuwa kitovu cha furaha, kumbukumbu, mawaidha na ujumbe wa upendo katika hafla hiyo adhimu ya Maulidi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha